Nini maana ya kupanga mikakati?

Nini maana ya kupanga mikakati?

Kupanga Mikakati Ni (1) Kushughulikia Madhaifu Yako Ili Kukabiliana Na Madhara Yanayoweza Jitokeza Na (2) Kupembua Umahiri Wako Ili Kuzinyakua Fursa Zote Zilizombele Yako. Swala la kupanga mikakati wazungu huliita strategic planning. Ni jambo muhimu sana kwa kila mtu kulifanya hata kama haupo kwenye biashara. Ni muhimu kupanga mikakati kwakuwa kila mtu ana madhaifu yake, kila mtu anakabiliwa na madhara ya aina yake, kila mtu ana kipawa chake, na kila mtu ana fursa zake. Kupanga mikakati kuna hatua sita muhimu.

(1) kuorodhesha madhaifu yako yote (weaknesses).
Kumbuka kuwa madhaifu hatuongelei yale tu ya kibiashara la hasha bali ni kila aina ya udhaifu ulionao. Mfano kuna watu wanapata hasira kwa haraka. Kuna watu hawana afya madhubuti. Kuna watu hawana pesa za mitaji. Kuna watu hawana uwezo wa kuchangamana na watu. Kuna watu ni wapole sana. Kuna watu ni wakorofi sana. Kuna watu hawana mbinu za biashara. Kuna watu hawana elimu. Kuna wenye elimu ya darasani ila hawajelimika. etc etc. Hata miamia tuna madhaifu yetu mojawapo likiwa kutokuwa na rasilimali za kutosha kuwafikia watu wengi zaidi katika kutoa elimu yetu.

Pamoja na kwamba kuna fursa ya kuendesha semina na mihadhara ila udhaifu uliopo ni kwamba hatuna muda wa kutosha kujigawa katika kila jambo. Hata tovuti yetu ya miamia.co.tz haiwekewi makala kila uchao kwa udhaifu wa kukosa muda na raslimali za kutosha. Hata muasisi wa miamia ndugu Juma Kessy ana madhaifu yake lukuki. Ukiona list ya madhaifu yake unaweza changanyikiwa. Ila bahati nzuri madhaifu yake yameorodheshwa na mbinu za kuyakabili. Sasa kwa wewe unaesoma makala hii ambae hujaorodhesha madhaifu yako hebu chukua kalamu na karatasi uanze kuyaorodhesha. Kuorodhesha madhaifu yako sio udhaifu ila kutoyaorodhesha ndio udhaifu.

Vyote kwa vyote ni kwamba kila mtu ameumbwa na madhaifu yake. Wakati mwingine inabidi uwazulize watu wako wa karibu wakwambie una madhaifu gani mengine ya ziada ambayo wewe mwenyewe hujaweza kuyaona. Hakikisha orodha hii umeiandika na hakikisha hauachi hata udhaifu mmoja ulionao. Hata mjamaa kutoweza mkabili mdada na kumweleza unavyomhusudu pia ni udhaifu na usiusahau kuuorodhesha.

Kuorodhesha madhaifu itakusaidia katika hatua ya tano hapa chini ambapo kwa kila udhaifu inatakiwa sasa uorodheshe mbinu ya kuukabili ili usijepatwa na madhara kutokana na udhaifu wako. Hata kijana kuwa legelege ni udhaifu na lazima upange mbinu za kuuondoa mana ikitokea siku familia yako ikawa hatarini mwanamke na watoto watategemea wewe ndio usimame kama baba.

(2) kuorodhesha madhara yanayoweza jitokeza kutokana na madhaifu uliyonayo (threats).
Mfano kwa kijana legelege siku mpo bichi na manzi wako afu gafla unamuona anazama kwenye maji hapo lazima ujue kuogelea kumuokoa. Na kama kuna mbabe anataka kuwapiga lazima uwe imara kujitetea na kumtetea manzi wako.

Huna kazi, huna mtaji na unategemea wazazi ama mwanaume wako jua wazi wakitoweka utabaki hohehahe. Una biashara na hutunzi kumbukumbu jua wazi madhara yanayoweza jitokeza ni mali kupotea bila habari. Kila udhaifu unapelekea kuwepo kwa madhara yanayoweza jitokeza. Hakikisha umeyaorodhesha yote.

(3) kuorodhesha mambo na maeneo yote ambayo una umahiri nayo na yale ambayo wewe umebarikiwa wengine hawakubarikiwa (strengths).
Hapa napo orodhesha vipawa vyako vyote na yote yale ambayo umebarikiwa nayo. Kila kipawa na baraka uliyonayo inaweza kusaidia kutwaa fursa flani iliyombele yako. Una kipaji cha kucheza mpira basi kuna fursa mbele yako.

Una kipaji cha kuchekesha basi kuna fursa mbele yako. Umebarikiwa uwezo mkubwa wa kiakili basi kuna fursa mbele yako. Umebarikiwa uzuri wa sura na umbo basi kuna fursa mbele yako. Umebarikiwa uwezo wa kukimbia sana basi kuna fursa mbele yako. Umebarikiwa uvumilivu basi kuna fursa mbele yako. Una ajira basi kuna fursa mbele yako. Una elimu basi kuna fursa mbele yako. Umkakamavu basi kuna fursa mbele yako. etc etc. Usisahau kuorodhesha hata kipawa kimoja ulichonacho ama ulichobarikiwa.

(4) kuorodhesha fursa zote unazoweza zinyakua kwa kutumia umahiri ulionao (opportunities).
Sasa kama una umahiri na kipawa flani na hujui fursa gani unaweza zinyakua kwa kutumia umahiri huo ama kipawa hicho basi hapo umekwamia pabaya. Kaa chini orodhesha fursa zote ambazo unaweza zinyakua kwa kutumia umahiri na kipawa ulichonacho. Ukishaorodhesha fursa nyingi kilichobaki ni kuweka mbinu na vipaumbele kama inavyoelezwa namba sita hapa chini.

(5) kwa kila aina ya udhaifu ulionao orodhesha mbinu mbalimbali zinazohitajika ili kurekebisha udhaifu huo.
Hii itasaidia kuweza kujiondoa katika uwezekano wa kukumbwa na madhara yatokanayo na udhaifu wako. Mfano nikiwa shule ya msingi kuna jamaa walikuwa wakinionea sana nilipofika kidato cha kwanza nikaona kuna haja ya kuingia jim na kujifunza kupigana.

Niliporudi likizo jamaa mmoja akanikabili akidhani ni yule kibonde wake wa enzi zile. Nikamnyoosha haswa. Weka mbinu za kuyakabili madhaifu yako yote. Huna mtaji wa biashara tafuta ajira ya aina yoyote ile hata kama wenzako wanaidharau. Kusanya pesa polepole. Huna elimu weka mbinu za kujifunza. Una ajira ila baadhi ya kazi hujui namna ya kuzifanya nenda vyuo vya jioni kasome. Una biashara ila huna huna ari ya kutunza kumbukumbu weka mbinu za kukabiliana na hili suala. Biashara inayumba kwa kuwa na udhaifu wa kushindwa kusimamia vyema tafuta washauri. etc etc.

(6) kwa kila jambo ama eneo ambalo una umahiri nalo orodhesha mbinu za kutumia umahiri huo kujitwalia fursa zote zilizo mbele yako.
Fursa ulizoziorodhesha katika hatua ya nne lazima utumie umahiri na kipawa ulichonacho na yale uliyobarikiwa kuzitwaa. Una elimu na kazi zinatangazwa kila leo ila ukiomba hata kwenye usaili huitwi. Unajua nini sababu? Hujapanga mbinu za kuitwaa hiyo fursa ya ajira. Kuajiriwa sio cheti tu. Ni pamoja na umahiri wako wa kuyaendea mambo.

Hata barua yako ya maombi ya kazi inaweza muonesha mtu kuwa unajielewa ama hujielewi. Jifunze kuandika proposal. Jifunze kupembua eneo ulilobobea. Unajua muajiri hatafuti vyeti bali anatafuta kipawa. Dhihirisha kipawa chako kwenye barua ya maombi na kwenye usaili. Ukikwama karibu miamia tukusaidie. Tembelea miamia.co.tz/english ama miamia.co.tz/swahili kwa mawasiliano. #MiaMiatz #KukuzaMaarifa #KuongezaUstawi

About Juma Kessy 49 Articles
Napenda sana ujasiriamali. Napenda vijana wote wajue kanuni muhimu za ujasiriamali. Msingi unaoniongoza ni maarifa kwa wote. Na lengo langu kuu ni Kukuza Maarifa na Kuongeza Ustawi.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*