Ujasiriamali ni wajibu sio zawadi

Kuna kauli huwa watu wanaziongea kana kwamba wakiingia kwenye ujasiriamali ndio matatizo yao ya kifedha yatakuwa yamepata ufumbuzi. Sio mbaya kuwaza hivyo ila niwakumbushe tu unapoanza kuingia kwenye ujasiriamali usiingie kama unaingia kwenye sherehe ya kujipongeza bali ingia kama askari alieingia uwanja wa vita.

Najua watu hawapendi makala zenye kuwaeleza ukweli ila bora uujue ukweli kuliko uingie bila kujipanga kuyakabili haya mambo.

Ukiingia kwa fikra kwamba kujiajiri ndio jambo litalotatua matatizo yako yote ya kifedha sio jambo jema mana unaweza poteza muelekeo katika uwanja wa mapambano (uwanja wa ujasiriamali).

Unajua kwanini ujasiriamali ni jukumu na sio zawadi? Kuna sababu kadhaa.

1. Mara nyingi masaa ya kazi huongezeka. Mjasiriamali mara nyingi hufanya biashara zake kwa matumaini wateja watajitokeza mda si punde. Hii humfanya aendelee kusubiri subiri na hatimae muda huenda. Mtu alieajiriwa kwenye idara na taasisi za uma anajua kuwa wikiendi inaanza ijumaa jioni ila aliejiajiri wikiendi hufutika kabisa na kama ikibaki basi ni jpili tu.

2. Ujasiriamali unaweza pelekea ukawa huna likizo iwe ya muda mfupi ama muda mrefu. Wapo wanaojipa likizo ila mwanzoni unapoanza mara nyingi wewe ndio unakuwa mmiliki na meneja wa biashara yako hivyo kupelekea kutoweza kuondoka mana unakuwa na tahadhari kwamba unaweza kuondoka huku nyuma mambo yakayumba. Ijapokuwa hii hutegemeana na aina ya biashara na jinsi ulivyoipangilia.

3. Mapato yako hayawi fixed kama yale ya ajira. Kwenye ujasiriamali mapato yanapanda na kushuka kutegemeana na mwenendo wa soko.

4. Ujasiriamali huhitaji ubunifu, utashi, ujuzi, kujiamini, na uwezo wa kujipanga na kupangilia mambo. Ni ngumu sana kuwa nayo haya yote hivyo basi ni ngumu sana kutabiri kuwa utafanikiwa ama utafeli kwenye ujasiriamali.

Ili kuepuka uwezekano wa kujikita matatani katika ujasiriamali tafakari haya:

1. Je una msukumo unaokusukuma kila saa kufanya biashara?

2. Je una nidhamu thabiti ya pesa?

3. Je una utashi na ujuzi wa kuifanya biashara unayoiendea?

4. Je familia yako inakuunga mkono kwenye wazo lako la biashara?

5. Je unaweza kumudu kuishi maisha yenye kipato kilicho chini kwa muda?

6. Una utashi wa kuongoza watu?

7. Unajua kutunza kumbukumbu za hesabu za fedha?

Kama kuna jambo hulijui katika haya hebu jaribu kuomba msaada upate japo training ama seminar upigwe msasa. Kujifunza mambo haya pia ni uwekezaji. Pesa unayoitumia kujiongezea maarifa haijapotea bure. #miamiatz #KukuzaMaarifa #KuongezaUstawi

About Juma Kessy 49 Articles
Napenda sana ujasiriamali. Napenda vijana wote wajue kanuni muhimu za ujasiriamali. Msingi unaoniongoza ni maarifa kwa wote. Na lengo langu kuu ni Kukuza Maarifa na Kuongeza Ustawi.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*