Fursa za mtaji wa laki moja (100,000) kwa wajasiriamali wadogo

Laki moja naweza kufanyia biashara gani?

Fursa za laki ni nyingi sana kwa alieamua kutoka ndani na kuingia mtaani. Kabla hujaendelea naomba nikupe angalizo.

Kama hujaamua kutoka ndani na kuingia mtaani ama kwa lugha nyengine kama hujaamua kufuta aibu kichwani mwako basi hii makala haikufai.

MAMA NTILIE, KIJIWE CHA CHIPS, KIJIWE CHA SUPU, KIJIWE CHA NYAMA CHOMA & MISHKAKI, KIJIWE CHA PWEZA, KIJIWE CHA MATUNDA (MATIKITI YA KUCHONGA), ETC

Kwa kawaida kila penye watu wengi ambao huwepo kwa muda mrefu basi pana wateja wa aina 2. Wa kipato kikubwa na kidogo.

Maeneo mengi yenye watu wengi panakuwa na migahawa kadhaa. Mathalan kwenye mahospitali makubwa kama muhimbili, kwenye vituo vikubwa vya mabasi kama ubungo, kwenye viwanja vikubwa kama taifa, etc.

Humu kote kuna migahawa. Unachopaswa kufanya ni kuangalia je hisi sehemu zinapatikana milo ya kimaskini? Assume mtu ana nja na bajeti yake ni 1000 tu je unaweza kumuuzia chakila kwa bei hiyo?

Wengi wa hawa wa bajeti za chini wanachoangalia zaidi ni chakula kisafi cha kushiba. Hawana mbwembwe ya mboga mbili tatu. Hata kama ni wali maharage ni sawa tu ilimradi iwe katika bajeti yake.

Makala hii itaendelea. Tutapitia fursa nyingi sana za mtaji wa laki moja. Usikose kuendelea kufuatilia ukurasa huu.

Nini cha kufanya kama una mtaji zaidi ya laki

Kwanza niwashukuru kwa dua zenu. Pia shukrani za pekee ziende kwa ndugu Eliud Msofe ambae kwa sasa yeye ndio ameshika usukani wa miamia.

Hata hizi makala mimi ni mtoa idea yeye ndio muwasilishaji kwa maana ya kuziweka idea katika maandishi.

NINI CHA KUFANYA KWA WENYE MITAJI MIKUBWA?
Kabla ya kuendelea na zile fursa za biashara za laki moja nimeona nitoe angalizo kwa wale wenye mitaji mikubwa kiasi.

Ukiwa na mtaji mkubwa kiasi haina maana kuwa ndio ujiingize ktk idea kubwa kubwa. Bali ingia kwenye idea ndogo ndogo na uzifanye kwa ukubwa.

FAIDA YAKE
Faida ya huu mtindo ni kwamba unaweza kuisoma biashara na kuiteka gafla. Mfano ni mtindo anaoutumia Baressa kuzichukua idea ndogo na kuzifanya kwa ukubwa.

Tumeona ice cream, tumeona juice, tumeona ukwaju, tumeona karanga, tumeona ubuyu, na kadhali na kadhalika.

MFANO
Labda wewe una milioni kumi ama zaidi na unawaza biashara ya kufanya. Unaweza ukachukua idea hizi za laki ukazifanya kwa ukubwa zaidi kama anavyofanya Baressa.

Tuchukulie umeamua kuifanya ile ya mayai. Utakachokifanya ni kuifanya kwa kiwango cha kisasa na kikubwa.

Wale vijana kwako watakuwa mawakala. Mtaingia mikataba. Utawapa tisheti. Utawapa kiwango wanachotakiwa kuuza kwa siku. Utawapa mafunzo ya ujasiriamali na utawalipa commission. Watauza kama wale wa Baressa wanavyouza ukwaju.

Inatakiwa pia kujenga brand mitandaoni. Hakikisha unakuwa na posts nyingi sana zinazoongelea biashara hii. Usione hasara kuwa na camera man wako maalum kwa siku awe anapiga picha za kutosha na ku edit.

ANGALIZO
Biashara ndogo ni nyepesi wengine kuiga hivyo unatakiwa kuwa na ubunifu wa ziada. Kila mara kaa na watu unaoamini kuwa wana ubunifu na wakupe maoni yao.

Bahati mbaya sana watanzania tukishasimama katika biashara tuna ignore kutafuta ushauri mpaka tuanguke.

Ukiwa karibu na wabunifu ni rahisi kutumia hili gurudumu kupanua wigo wako kila mara kuliko kusubiri wengine waige na kuanza kulalama.

Fursa namba moja ya mtaji wa laki moja

Mradi wa kwanza wa laki moja ambao nitauzungumzia ni wa biashara ya mayai ya kuchemsha. Mradi huu utakuhitaji kuajiri kina/binti mmoja au zaidi kulingana na upatikanaji na uaminifu wa vijana ambao unahisi watakufaa.

Katika mfano wangu ambao nitatumia eneo la dar:

1. Nita ajiri vijana watatu ambao nawafahamu mwenendo wao.

2. Nitanunua mayai trey 9 pamoja na trey zake. Hapa nitatumia kati ya 70,000 hadi 90,000.

3. Nitanunua chumvi pakti moja.

4. Nitachemsha hayo mayai trey zote 9.

5. Kila kijana ataondoka na trey tatu asubui na kwenda kuuza maeneo ya mchanganyiko ikiwa either ni stendi na sehemu kama hizo.

6. Makubaliano kwa vijana hao watatu ni kwamba kila trey ambayo mtu anauza nitamlipa shilingi 3000. Na bei ya yai wanapaswa wauze shilingi 500.

7. Mapato kwa siku ya kwanza yatakuwa 500x30x9 = 135,000. Kati ya hizo nitawapa vijana shilingi 9,000 kila mmoja.

8. Ratiba itaendelea hivyo kwa muda na nitapanua biashara itakapobidi.

Gharama zingine ndogo ndogo ni kama mkaa na chumvi na ni kiasi kidogo sana.

Hivyo gharama zetu ni:
Mayai na trey zake = maximum 90,000
Malipo kwa vijana = 27,000
Chumvi, mkaa = 3,000

Jumla 120,000.

Mauzo 135,000 toa gharama 120,000 sawa na faida 15,000. Kuanzia siku ya pili faida itaongezeka mana hatununui mayai na trey zake bali tunanunua mayai pekee.

Makala ambayo tunapendekeza uisome pia ni ile ihusuyo utunzaji wa kumbukumbu katika ujasiriamali. Bofya hapa kuisoma.

Fursa namba mbili ya mtaji wa laki

Fursa ya pili ya laki moja ambayo nitaizungumzia ni biashara ya genge. Genge ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mitaani. Wachache sana huku mitaani kwetu ambao huenda shopping ya kujaza vitu ndani.

Wengi wetu hununua mahitaji ya papo kwa papo. Hebu toka tembea tembea na uangazie mazingira ya mitaani kwenu, mitaa ya jirani, mitaa ya mbali kidogo, mitaa ya sokoni, etc.

Katika tembea tembea yako angalia ni wapi pana uhaba wa magenge. Na pia unapopita magengeni angalia viashiria vya soko kuwepo. Ukipita sehemu ukaona watu husubiria kuhudumiwa mmoja mmoja na wapo wengi jua kuwa hapo kuna fursa kubwa sana.

Pachunguze na uorodheshe mambo ambayo kwako unaona ni mapungufu ya hilo au hayo magenge. Ukishaorodhesha mapungufu angalia na ubuni njia ya kuwa na genge ambalo litatoa nafuu kwa wateja.

VITU VYA MSINGI GENGENI
1. Mboga majani
2. Vingia mchuzi kama nyanya, carrots, hoho, vitunguu, etc
3. Viungo vya ziada kama iliki, dalasini, swaumu, etc
4. Matunda kama tikiti, tango, chungwa, papai, parachichi, embe, nanasi, etc
5. Viazi, nazi, ndizi mbichi, etc

NJIA ZA KUJUA FAIDA
Kupata urahisi orodhesha hivi vitu katika karatasi ya shopping na uweke idadi. Ukimaliza pita magenge kadhaa na ukifika uliza bei ya vitu hivyo na uinakili.

Ukimaliza nenda sokoni wanapouza bidhaa hizo bei za jumla. Uliza bei na uorodheshe bei hizo.

Fanya hesabu katika laki moja utaanza na idadi gani ya vitu gani mana hutomudu kuweka kila kitu kwa laki moja ila pia hutokosa soko hata kama utakuwa na vitu vya elfu 20.

Ukishamaliza hesabu za hapo juu linganisha jumla ya pesa utayotumia ukinunua vitu hivyo kwa bei ulizoona sokoni na jumla ya mapato utayoyapata ukiuza bidhaa hizo. Tofauti yake huwa ni faida yako.

KWA MFANO
Kwa kawaida sado moja ya viazi utauziwa kati ya 3,000 hadi 4,500 kulingana na sehemu. Tathmini kadhaa zilizofanyika zinaonesha kuwa sado moja huingia wastani wa mafungu 9.

Kuna baadhi ya sehemu mafungu hayo wanauza kwa 500 na sehemu nyengine wanauza kwa 1000.

Ukinunua sado moja kwa 3,000 ukauza fungu kwa 500 na ukapanga fungu 9 utapata 4,500. Hapa faida ghafi ni 1,500.

Ukinunua kwa 4,500 ukapanga fungu 7 na kila fungu ukauza kwa 1,000 utapata 7,000. Hapa faida ghafi ni 2,500.

Kwa ufupi katika biashara ya genge katika kila 10,000 unayoingiza faida chache sana utayoipata ni 2,500.

Sasa kazi ni kwako kuangalia sehemu yenye mzunguuko mzuri. Ukiuza bidhaa za 60,000 kwa siku utapata zaidi ya 15,000 faida kwa siku.

Usiache kutufuatilia facebook.com/miamiatz kwa fursa mbalimbali na uhamasishaji mbalimbali.

Fursa namba tatu ya mtaji wa laki moja (100,000)

Fursa ya tatu ya laki moja ambayo nitaizungumzia ni biashara ya matunda. Biashara hii hufanyika kwa matunda mazima na yale ya kukata.

Matunda muhimu ambayo kwa siku unaweza kuwa na uhakika wa kulala na faida isiyopungua 15,000 ni:

1. Matikiti
2. Mapapai
3. Maparachichi na
4. Machungwa.

Kuna matunda mengine ya kupambia biashara yako ila hayo hapo juu ni yale ambayo biashara yake ni uhakika zaidi.

UNAPATAJE SEHEMU YENYE UHAKIKA WA KUUZA?
Jaribu kupita pita mitaa ya watu wengi iwe ni karibu na unapoishi ama hata kama ni mbali na hapo. Biashara hii inafaa zaidi sehemu ambazo watu wengi hupita wanaporejea majumbani kwao.

Itafaa zaidi kama itakuwa ni karibu na kituo cha mwisho cha daladala ambapo watu wakishuka huelekea majumbani kwao. Ama maeneo ya mahospitali makubwa sehemu ambapo watu hupitia kuingia ama kutokea hospitali. Na sehemu za vituo vya dala dala vikubwa.

Ukipata sehemu ambapo tayari kuna wauzaji wengine ni vyema zaidi mana ni ishara kuwa pana mzunguuko mzuri. Ongea nao kistaarabu uwadadisi.

Njia bora siku zote ya kupata taarifa za biashara ni kwa kuanza kuwa mteja. Mfanya biashara atakuwa rafiki yako kama utaanza kwa kumuungisha kwanza.

KUNA JAMBO WENGI WETU HATULIJUI, SOMA HAPA
Kwa kawaida mtaji wa biashara huanza kufanya kazi siku unapoamua kuanza kufuatilia hiyo biashara. Kuna gharama utaingia ikiwemo kulichunguza soko. Nauli za hapa na pale.

Wakati mwingine hata washauri nao watataka uwatoe chochote. Kumbuka siku zote cha bure huwa hakiwi kamili. Ukiona kuna jambo limekushinda ukahitaji msaada wa mtu basi jua kuwa kuna shukrani lazima uoneshe.

Hivyo basi gharama zote za kufuatilia jambo lako mpaka ukapata maelezo ya kutosha kuanza biashara yako lazima ziwe sehemu ya ile laki ya mtaji tunayoiongelea. Na hii ni kwa mtaji wowote ule hata kama ni zaidi ya laki.

NJIA ZA KUJUA FAIDA UTAYOIPATA
Ili kujua faida gani utaipata kwa kila aina ya tunda fanya hivi:

Pitia kwa muuzaji wa matunda. Angalia bei ya wastani ya hayo matunda. Kama anakata na unapanga nawewe kukata mfano matikiti hebu angalia akianza kukata tikiti anatoa vipande vingapi vya bei gani.

Mfano tikiti la elf5 sokoni linaweza kukatwa vipande 8 vya 200, vipande 6 vya 500 na vipande 4 vya 1,000. Hii ina maana kila tikiti litatoka vipande 17 vya saizi tofauti tofauti na bei tofauti tofauti na jumla utapata faida ghafi 3,600.

Ukiweza kuuza vipande 50 kwa siku ni sawa na wastani wa matikiti matatu. Faida itakuwa 10,800 kutoka kwenye matikiti matatu pekee.

Bado una maparachichi, mapapai na machungwa. Kiufupi huwezi kosa 20,000 ya faida kwa siku. Kwa mwezi utakuwa na angalau 500,000 kwenda juu ya faida.

VIFAA VYA BIASHARA
Vifaa vya biashara ikiwemo meza, stuli, kipande cha turubai ikilazimu ama mwamvuli, visu, ndoo, nakadhali vinapaswa kutoka katika mtaji huo huo.

Ukiongea vizuri na waliopo kwenye biashara hii utapata maarifa zaidi juu ya vifaa na njia sahihi ya biashara.

Cha msingi ni wewe kutoka nje usijifungie ndani ukataka kila kitu ujulie kwenye simu tu. Kuna baadhi ya vitu lazima upite mtaani. Na kama wewe ni mtu wa aibu sana basi inabidi upate njia ya kuweka pembeni aibu kwanza.

MWISHO
Sana kazi ni kwako kuangalia sehemu yenye mzunguuko mzuri. Kumbuka mali bila daftari hupotea bila habari. Pia kumbuka mteja namba moja ni wewe mwenyewe, usile kitu cha bure kwenye biashara yako. Lipia kila unachochukua.

SOMA HIZI PIA

  1. Biashara ya mtaji wa laki mbili (200,000)
  2. Biashara ya mtaji wa laki tatu (300,000)

Imeandikwa na Kessy Juma

Kessy Juma Kessy Juma is the founder of Miamia Trading Company (miamiatz). He is a Techpreneur with roots in accountancy. I believe any business is good as long as the owner is passionate, does proper research, collects proper data and does proper analysis.

miamia miamia miamia miamia
Was this page helpful?
YesNo
Scroll to Top